KUHUSU
Eneo la mashariki mwa Bonde kubwa la Congo, ambalo kiutamaduni linatafautiana vizuri sana, linakaliwa na watu wa makabila yasiyofahamika kwa urahisi. Kwa kujipatia chakula, makabila haya yanatumia mbinu zenye kutegemeana. Miongoni mwa lugha zao, kuna zile zinazokuwa katika makundi mengi madogo ya asili ya kibantu, ya kiubangui ao ile ya kisudani ya kati. Historia ya eneo hili inapashwa kuwa ya kuvutia sana : makabila haya yalitokea wapi ? Ni wakati gani yaliweza kukutana ? Ni aina gani ya mabadilishano ya vitu yaliweza kufanyika kati yao ?
Tangu sasa kuna watafiti wachache waliotupia macho yao kwenye nyakati za zamani sana za historia ya eneo linalopatikana kandokando ya Kisangani. Mradi BANTURIVERS ni jopo linalotungwa na wataalamu wa sayansi nyingi juu ya kutaka kuandika historia ya kukaliwa na watu eneo hili. Na kwa kuwa kilimo ni kigumu kufanyika katika mazingira ya msitu wa Ikweta, BANTURIVERS inajishurlisha, pia, na kazi za mito kama njia za kupitia ndani ya msitu na kama nafasi nyingi za kujipatia chakula cha protini (kutoka kwa samaki).
ISIMU
Wakitegamia maneno, sauti na mofimu za lugha za kisasa kama funguo kwa kuingilia katika nyakati za kale, wanaisimu wanajifunza asili na njia zilizofwatwa na majamii ya kwanza ya kilugha katika eneo la mashariki mwa Bonde kubwa la Congo, mabadilishano ya vitu kati ya majamii tofauti, ukuaji wao, pamoja na ginsi majamii haya yaliweza kupata umaarufu katika mbinu za uvuvi na zile za kusafiri kwenye mito.
ANTHROPOLOJIA
Haiwezekani kuelewa nyakati za kale bila kuelewa nyakati za sasa. Ndiyo sababu wanaanthropolojia watafanya tafiti kuhusu matumizi siku hizi ya mito katika Bonde kubwa la Congo, ni kusema kuhusu : mbinu za uvuvi na usafiri kwenye mito, kazi ya wavuvi katika mitandao ya kibishara ndani ya eneo hili, na vilevile ulimwengu wa alama za maisha kandokando mwa jito.
ARKEOLOJIA
Wanaarkeolojia watakusanya data za nyakati za sasa na zile za zamani. Mahojiano na wanawake wafinyanzi wa vyombo, hawa wakiwa, mara nyingi, wale wa majamii ya wavuvi, yataleta taarifa kuhusu mbinu za ufinyanzi wa vyombo na zile za mitandao.
Sibitisho za moja kwa moja za kuweko utamaduni wa zamani wa kivyombo zitatolewa na masalio ya hapo mwanzo kwenye kandokando mwa jito Congo na kwenye mito yake inayoliongezea maji, kunako eneo kati ya Bumba na Kindu.
BANTURIVERS, ni nini ?
Mradi BANTURIVERS unachunguza kipindi kimoja kisichojulikana juu ya kusambaa Wabantu, ukitegemea mbinu moja ya kujipatia chakula ambayo historia yake inajifunzwa mara haba: matumizi ya MITO. Mradi huu unapatikana katika eneo la mashariki mwa Bonde kubwa la Congo, njia panda ya lugha na tamaduni.
Nyakati za kale za Afrika ya kati, mbele ya kipindi cha Ukoloni, ni sawa na msitu wa Ikweta unaopatikana katikati yake. Kwa mtazamo wa kwanza, historia ya zamani sana ya eneo hili inaonekana kutoeleweka kwa sababu ya ukosefu wa maandishi ya kabla ya kuweko mahusiano na Wazungu na Waarabu, na pia kutokana na hali ya mazingira ambayo hairahisishi kufanyika tafiti za kiarkeolojia.Tangu sasa, kwa kuwa mito inawezesha kuingia katika msitu, methodolojia fulani zinawawezesha watafiti kujipenya katika nyakati za kale na kugundua zaidi sehemu mbalimbali sana za historia zilizojipanga kwa daraja. Wataalamu wengi : wa isimu, wa arkaelojia, wa historia, wa sayansi za urisi wa viumbe, wale wanaoshurlika na hali ya mazingira katika nyakati fulani, pamoja na watafiti wengine wa sayansi tofauti wanajihusisha na tafiti kuhusu « kusambaa kwa Wabantu ». Jambo linaloambatana na ulizo ni kwamba ni ginsi gani kundi kubwa la lugha (kati ya 400 na 600 lugha), linaloangaliwa kama kundi moja ndogo tu la tawi la Niger-Congo, liliweza kutawanyika kunako nusu ya bara nzima la Afrika (kutoka Kameruni mpaka kusini mwa Somalia na hadi Afrika ya kusini) mnamo kipindi kimoja kifupi sana (cha milenia chache tu ). Labda kusambaa huku kuliweza kuambatana na uhamiaji wa watu; na hata pia kama kungeliweza kufanyika kwa aina nyingine za kusambaa lugha, kwa mfano kutokana na mabadiliko ya lugha. Yote hii iliweza kuchangia katika kusambaa Wabantu. Tafiti nyingi juu ya kusambaa Wabantu zinawakusanya wataalamu mbalimbali. Hawa wanashurlika tu na kule kusambaa kwa mwanzo kwa majamii ya kwanza ya Wabantu na wanajulisha njia zilizofwatwa na Wabantu wakizunguuka msitu wa Ikweta. Makabila ya kwanza yaliyokuwa yakizungumza lugha za kibantu yalikuwa ni ya walimaji. Kilimo kilikuwa ni moja ya njia zao za kujipatia chakula. Kwa hiyo, majamii haya yalipendelea kuishi kwenye savana. Wakati mabadiliko ya hali ya nchi yalifungua njia kunako msitu, makabila ya Wabantu yaliweza kuishi kunako savana za pembeni ya Kameruni ya kati na ya Gaboni, mnamo karibuni myaka ya 4000 BP. Mnamo karibuni myaka 2500 BP, mlango wa savana « savannah corridor », kandokando ya mto Sangha uliwawezesha « Wabantu walimaji » kuhamia kunako sehemu za kusini, wakizunguuka msitu mpaka kufikia kwenye savana za kusini (p.ex. Bostoen et al. 2015). Sasa, wakati moja, hali ya nchi iliweza mara tena kubadilika na msitu kurejea kama hapo mwanzo. Hii haikutokana na kugawanyika kati ya majamii ya Wabantu kaskazini na wale wa kusini mwa msitu. Lakini wazungumzaji wa lugha za kibantu walizidi kwenda kunako msitu ; na sasa lugha zao ni sehemu moja kubwa ya lugha zinazotawala kwenye msitu wa Ikweta, katika Afrika ya kati. Na kwa kuwa kilimo ni kigumu kufanyika katika msitu wa Ikweta, ni nini, basi, iliyorahisisha majamii ya Wabantu kuishi katika msitu huu ? Vansina (1990) analipatia umuhimu mkubwa jambo la kuingizwa aina moja ya mgomba katika maeneo hayo. Lakini, migomba, viazi, na vyakula vingine vyenye uwanga vina protini ndogo tu katika msitu wa Ikweta. Na tena, kwa kuwa ufugaji wa nyama ni mdogo katika mazingira ya Tropiki, kilimo kinapashwa kutegemea mbinu za ukusanyaji vyakula, kwa mfano, kuwinda wanyama, kuogota vidudu na pia kazi ya uvuvi. Katika Afrika ya kati, siyo tu mimea mingi inayotawala kwenye ramani zake zilizochorwa kwa njia ya sateliti, bali kuna pia mito mingi mahali pote ndani ya msitu wa Ikweta. Na kwa msaada wa mito yake mingi inayoliongezea maji, jito Congo linachukua nafasi ya pili duniani, kisha jito Amazoni, kwa nguvu ya mkondo wa maji yake. Ni hivi Vansina anaamini ya kwamba mito katika Bonde kubwa la Congo ilitumika kama « njia » za kusafiria katika msitu. Hakika, sehemu kubwa za jito Congo na zile za mito mingi inayoliongezea maji zinaweza kusafiriwa. Na siku hizi sehemu hizi, katika maeneo haya, zinatumiwa, mara nyingi, kama njia bora za uchukuzi wa vitu na watu. Sibitisho za kwanza za kiarkeolojia zinahakikisha kuweko uhamiaji moja wa rafla wa watu kandokando mwa jito ambao unaweza kueleza ginsi gani watu walilikalia eneo linalopatikana kati ya Pool Malebo na Kisangani (Wotzka 1995 ; Livingstoine-Smith et al. 2016). Pengine kusambaa huku kwa rafla kuliweza kuambatana na kutegemea sana mazao ya majini. Ni hivi BANTURIVERS inatilia sana mkazo upande wa mito katika historia : mito kama njia ao kama vizuizi kwenye sehemu za maporomoko ; lakini hasa zaidi kutokana na uzoefu wa majamii tofauti ya zamani juu ya kuishi kwenye kandokando ya mito. Tunapendelea kujifunza kwa undani orodha ya makabila tofauti ya zamani ya Wabantu, kandokando mwa mito. Mada yetu inahusika na usafiri wao kwenye mito, uvuvi na mapishi ya samaki, lakini, pia na maswali ya tamaduni za kijamii na maisha kandokando mwa mito, biashara, jiografia ya vijiji na kazi pembeni ya mito.
Uwanja wa utafiti wa mradi huu ni eneo la mashariki mwa Bonde kubwa la Congo, hasa kabisa eneo la kandokando mwa Kisangani mpaka Bumba, chini ya jito Congo, na Kindu kunako sehemu ya juu ya Lualaba. Kiutamaduni, eneo hili ambalo ni tofauti sana linakaliwa na majamii yanayozungumza lugha zilizopangwa katika makundi madogo tofauti ya kibantu, na pia lugha nyingine sizisokuwa za kibantu. Majamii haya yanajitambulisha katika makabila yasiyofahamika kwa urahisi na ambayo, mara nyingi, yamegeuka maarufu katika mbinu zinazotegemeana kwa kujipatia chakula. Kufwatana na fikra za kisasa, eneo kandokando mwa Kisangani linaweza kuwa ni kituo cha mwisho kwa njia nyingi za uhamiaji. Makabila yenye tamaduni tofauti yalipashwa kujizoesha na hali ya mazingira ya mahali pale. Bila shaka, makabila haya yaliweza, vilevile, kubadilishana mbinu na ujuzi wenyi manufaa. BANTURIVERS inachunguza ni ginsi gani eneo la mashariki mwa Bonde kubwa la Congo liliweza kukaliwa na watu (watu gani, walifika wakati gani na walitokea wapi ?) na vilevile ni ginsi gani majamii haya yalijipatia sifa za pekee katika ufundi na mbinu zilizoweza kupatana na maisha, kandokando mwa mito.
Références
Livingstone-Smith, A., Cornelissen, E., de Franquen, C., Nikis, N., Mees, F., Tshibamba Mukendi, J., Beeckman, H., Bourland, N. & Hubau, W. 2016. Forests and Rivers: The Archaeology of the North Eastern Congo. Quaternary International.
Vansina, J. 1990. Paths in the Rainforest. Toward a History of Political Tradition in Equatorial Africa. Madison: University of Wisconsin Press.
Wotzka, H.-P. 1995. Studien zur Archäologie des zentralafrikanischen Regenwaldes: Die Keramik des inneren Zaïre-Beckens und ihre Stellung im Kontext der Bantu-Expansion. Africa Praehistorica 6 – Cologne: Heinrich-Barth-Institut.